Kwa muda mrefu watu wengi wakazi wa kijiji cha Kipara wamekua na shauku au hamu kubwa ya kuona uwanja wa mpira wa Shule ya Msingi Mapinduzi ukijengewa aidha kwa hatua ya wigo wa mianzi au tofali, lakini changamoto kubwa ilikuwa ni namna gani ya kulifanikisha wazo hasa ukizingatia ni namna gani nzuri itatumika katika kulikamilisha wazo.
Changamoto ya tathmini ya gharama, umoja, wito na jiografia ya kiwanja kilipo karibu na barabara nazo zimekuwa changamoto kubwa zilizoumiza vichwa vya watu wengi lakini pia uduni wa utayari wa wamiliki kutoa kibali kwa wenye nia pia limekuwa tatizo sugu huenda lililochangia kusua sua kwa wazo lakini pia hata uzito wa mtoa wazo na namna unavyopokelewa na jamii husika kudharau hata kama hilo jambo linatekelezeka.
Kiu na shauku hiyo waliyonayo watu wengine ndiyo aliyokuwa nayo Mgao anapotamani siku moja ndoto yake inatimia ya kuwa na Kipara mpya yenye uwanja wenye hadhi angalau ya kuchezewa ligi daraja la pili kama sio la kwanza miongoni mwa viwanja ndani ya wilaya ya Nachingwea.
Ili kulifanikisha wazo, Mgao aliamini ili wazo likue lazima lipate lishe ya kulitetea kulipa nyama kwa watu waelezwe namna sahihi ya kufikia malengo na si kutoa tu ushauri wa tufanye, je tufanye kwa njia zipi.
Mwaka 2016 wazo liliwasilishwa kwenye kamati ya wajumbe wa kijiji katika waraka maalumu uliopewa jina la “USHAURI WANGU KWA SERIKALI YA KIJIJI/KATA KUHUSU MICHEZO KAMA SEKTA INAYOSHIRIKISHA VIJANA WENGI”
Kwenye waraka huo yalitolewa mapendekezo muhimu manne ya msingi na miongoni mwa mapendekezo hayo ni hili la Kujengea Uwanja kwa hatua ya kuta za tofali. Mapendekezo hayo yalikuwa kama hivi:-
1. Kuunda Idara ya Michezo au kamati kuu na kupewa jina maalumu itakayosimamia masuala ya michezo ndani ya Kata.
2. Serikali ya Kata/Kijiji kuandaa au kuanzisha ligi kuu endelevu ya ngazi ya Kata kila mwaka kama sehemu ya kipaumbele kwa vijana.
3. Kuujengea Uwanja wa mpira wa miguu.
4. Kuwa na siku maalumu ya Michezo yote itakayotengwa kwa mwaka kwa ajili ya Michezo, burudani au ya kitamaduni kwa ajili ya kudumisha mila.
Hayo yalikuwa mapendekezo makuu na kwa maelezo zaidi yamo katika andiko lake la Volume 3.
Mwaka 2016 wazo la kujengea kiwanja liliwasilishwa pia kwenye klabu ya Stone Fire FC kama chanzo kimojawapo cha mapato ya klabu na lilipokelewa kwa mikono miwili. Mwaka 2017 mwezi Aprili klabu ya Stone Fire chini ya mdhamini kocha Mkuu bwana Athuman Kadege walifanikiwa kuingia mkataba na shule ma kuujengea kwa wigo wa mianzi.
Baada ya hatua za awali kufanikiwa, mwaka 2017 mwezi Agosti, Mgao aliamua kuiendeleza kampeni hii na kuupa mpango maalumu wa kuhamasisha ujenzi wa uwanja kupitia wadau wenye moyo wa kujitoa kwa njia ya kuwekeza na kuupa jina linalojulikana kama “UWANJA WETU PROJECT”